Exodus 7:9-23

9 a“Farao atakapowaambia, ‘Fanyeni muujiza,’ basi mwambie Aroni, ‘Chukua fimbo yako na uitupe chini mbele ya Farao,’ nayo fimbo itakuwa nyoka.”

10Ndipo Mose na Aroni wakaenda kwa Farao wakafanya sawasawa kama vile Bwana alivyoagiza. Aroni akaitupa ile fimbo yake chini mbele ya Farao na maafisa wake, nayo ikawa nyoka. 11 bFarao naye akawaita watu wenye maarifa na wachawi na waganga wa Kimisri, nao wakafanya vivyo hivyo kwa siri ya uganga wao. 12Kila mmoja alitupa fimbo yake chini, nayo ikawa nyoka. Lakini fimbo ya Aroni ikazimeza zile fimbo zao. 13 cHata hivyo moyo wa Farao ukawa mgumu, naye hakuwasikiliza Mose na Aroni, sawasawa kama vile Bwana alivyokuwa amesema.

Pigo La Kwanza: Damu

14 dKisha Bwana akamwambia Mose, “Moyo wa Farao ni mgumu, anakataa kuwaachia watu kuondoka. 15Nenda kwa Farao asubuhi wakati anapokwenda mtoni. Ngoja ukingoni mwa Naili ili uonane naye, na uchukue mkononi mwako fimbo ile iliyobadilishwa kuwa nyoka. 16 eKisha umwambie, ‘Bwana, Mungu wa Waebrania, amenituma nikuambie: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu jangwani. Lakini hadi sasa hujasikiliza. 17 fHili ndilo Bwana asemalo: Kwa hili utajua kuwa Mimi ndimi Bwana: Fimbo iliyo mkononi mwangu nitapiga nayo maji ya Naili nayo yatabadilika kuwa damu. 18 gSamaki waliomo katika Mto Naili watakufa, nao mto utanuka vibaya, Wamisri hawataweza kunywa hayo maji yake.’ ”

19 h Bwana akamwambia Mose, “Mwambie Aroni, ‘Chukua ile fimbo yako unyooshe mkono wako juu ya maji ya Misri, juu ya chemchemi na mifereji, juu ya madimbwi na mabwawa yote,’ navyo vitabadilika kuwa damu. Damu itakuwa kila mahali katika Misri, hata kwenye vyombo vya miti na vya mawe.”

20 iMose na Aroni wakafanya kama vile Bwana alivyokuwa amewaagiza. Akainua fimbo yake machoni pa Farao na maafisa wake na kuyapiga maji ya Mto Naili, na maji yote yakabadilika kuwa damu. 21Samaki katika Mto Naili wakafa, nao mto ukanuka vibaya sana kiasi kwamba Wamisri hawakuweza kunywa maji yake. Damu ilikuwa kila mahali katika nchi ya Misri.

22 jLakini waganga wa Misri kwa kutumia siri ya uganga wao wakafanya vivyo hivyo, nao moyo wa Farao ukawa mgumu, hakuwasikiliza Mose na Aroni, kama vile Bwana alivyokuwa amesema. 23Badala yake, Farao akageuka, akaenda kwenye jumba lake la kifalme, wala hakulitia hili moyoni.
Copyright information for SwhNEN